Thursday, 26 September 2013

NI ARSENAL NA CHELSEA RAUNDI YA NNE KOMBE LA LIGI, UNITED NA VIBONDE NORWICH, NEWCASTLE NA MAN CITY

KLABU ya Arsenal itamenyana na wapinzani wao katika Jiji la London, Chelsea katika Raundi ya Nne ya Kombe la Ligi, maarufu kama Capital One Cup baada ya kuitoa West Brom kwa penalti 4-3 Uwanja wa Hawthorns.
Mechi hiyo imeisha kwa sare ya 1-1 usiku huu, lakini penalti walizokosa Morgan Amalfitano na Craig Dawson zinawasongesha mbele Gunners.


Mbele: United imesonga mbele kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Liverpool Uwanja wa Old Trafford

RATIBA KAMILI RAUNDI YA NNE CAPITAL ONE
Sunderland v Southampton
Leicester City v Fulham
Birmingham City v Stoke City
Manchester United v Norwich City
Burnley v West Ham United
Arsenal v Chelsea
Tottenham v Hull City
Newcastle v Manchester City
Mechi zote zitachezwa Jumanne ya Oktoba 29 na Jumatano ya Oktoba 30.
Manchester United baada ya kuwatoa wapinzan wao, Liverpool watamenyana na Norwich nyumbani katika Raundi ya Nne.
Bao pekee la Javier Hernandez mapema kipindi cha pili katika ushindi wa 1-0 Old Trafford, linawakutanisha Mashetani Wekundu na The Canaries Oktoba 28.
Birmingham iliyowatoa mabingwa watetezi Swansea kwa mabao 3-1 watacheza tena nyumbani katika 16 Bora, safari hii wakimenyana na timu ya Mark Hughes, Stoke.
Licha ya kupangiwa wapinzani wagumu, lakini The Blues bado wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa tena taji walilolitwaa mwaka 2011, na United ikiwa timu nyingine inayopewa nafasi pia baada ya kupangiwa Norwich.
Katika mechi nyingine, Newcastle itaikaribisha Manchester City Uwanja wa St James Park baada ya kuwatoa Leeds, wakati Hull wataifuata Tottenham siku kadhaa baada ya kucheza mechi ya Ligi Kuu, Uwanja wa White Hart Lane.
Timu isiyo na kocha kwa sasa, Sunderland itamenyana na Southampton, wakati West Ham watakwedna Kaskazini kumenyana na Burnley.
Fulham ya Martin Jol itaifuata Leicester kusaka nafasi ya Robo Fainali.
MIKWAJU YA PENALTI
West Brom: Reid (penalti ya kwanza) amefunga, Rosenberg amefunga, Morrison amefunga, Dawson amekosa, Amalfitano amekosa
Arsenal: Bendtner amefunga, Gnabry amekosa, Olsson amefunga, Akpom amefunga, Monreal amefunga
Arsenal imeifunga West Brom kwa penalti 4-3
Arsenal iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuitoa kwa matuta West Brom Uwanja wa The Hawthorns na kuingia Raundi ya Nne.
Eisfeld aliifungia Arsenal dakika ya 61 kabla ya Berahino kusawazisha dakika ya 71.
Kikosi cha West Brom kilikuwa: Daniels, Reid, Popov, Lugano, Dawson, Sinclair, Dorrans, Mulumbu/Morrison dk91, Berahino/Amalfitano dk101, Long/Rosenberg dk91, Sessegnon
Arsenal: Fabianski, Mertesacker, Vermaelen, Monreal, Jenkinson, Arteta/Bellerin dk95, Miyaichi, Gnabry, Hayden/Kris Olsson dk84, Bendtner, Eisfeld/Akpom dk82.



Ya ushindi: Nacho Monreal akiifungia Arsenal penalti ya ushindi

RONALDO APIGA ZOTE MBILI REAL IKING'ARA LA LIGA, BALE HAKUWEPO KABISAAA

PAMOJA na kumkosa mchezaji ghali duniani, Gareth Bale, lakini mchezaji anayeliwa mshahara mkubwa zaidi duniani, Cristiano Ronaldo alitosha kuipa pointi tatu Real Madrid usiku huu, baada ya kufunga mabao yote katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Elche.
Bale atarejea katika mechi ya nyumbani na Atletico Madrid Jumamosi wakati leo Ronaldo, ameendelea kuiweka Real karibu vinara wa La Liga.
Ronaldo alifunga mabnao hayo katika dakika za 51 na dakika ya sita ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90, wakati bao la kufutia machozi la Elche lilifungwa na Richmond Boakye dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimua dakika 90.
Kikosi cha Elche kilikuwa: Elche: Manu Herrera; Damián, Botía, Lombán, Albácar; Rubén Pérez, Carlos Sánchez; Stevanovic, Coro, Fidel na Boakye.
Real Madrid: Diego López, Pepe, Ramos, Coentrão, Khedira, Ronaldo, Benzema, Arbeloa, Modric, Di María na Isco.


Raha: Ronaldo akishangilia baada ya kuifungia Madrid bao la pili


Moja zaidi: Cristiano Ronaldo akishangilia na wachezaji wenzake


Weka kule: Real Madrid ilicheza bila mchezaji ghali duniani, Gareth Bale



Beki wa Elche, Botia (kushoto) akikabiliana na mshambuliaji Mfaransa wa Real Madrid, Karim Benzema

AKINA SAMATTA, ULIMWENGU WAANZIA UGENINI NUSU FAINALI AFRIKA NA MAZEMBE YAO

TOUT Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), itaanzia ugenini Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stade Malien ya Mali, Oktoba 6, mwaka huu, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Lubumbashi.
Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana, mchezo wa kwanza utachezwa kwenye Uwanja wa Modibo Keita mjini Bamako kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za huko na saa 12:00 kwa saa za Afrika Mashariki.


Mapacha watatu; Kutoka kulia Thomas Ulimwengu, Tresor Mputu na Mbwana Samatta washambuliaji hatari wa Mazembe ambao wanafunga karibu kila mechi

Mechi hiyo itachezeshwa na refa Alioum Neant, atakayesaidiwa na Evarist Menkouande wote wa Cameroon na Peter Edibi wa Nigeria, wakati refa wa akiba atakuwa Mohamadou Mal Souley pia wa Cameroon.
Timu hizo zitarudiana Oktoba 19, Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, zikichezeshwa na marefa Haimoudi Djamel wa Algeria atakayesaidiwa na Achik Redouane wa Morocco na Etchiali Abdelhak wa Algeria, wakati refa wa akiba atakuwa Bousseter Sofiane  wa Algeria pia.
Mazembe inayoongozwa na washambuliaji wawili wa Kitanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu, ikifanikiwa kuitoa Stade Malien itamenyana na mshindi wa Nusu nyingine, kati ya timu za Tunisia tupu, Club Africaine na C.S. Sfaxien.

Ikumbukwe Mazembe iliangukia kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na sasa inaelekea kufuta machungu kwa kutwaa taji hilo la pili kwa ukubwa kwa michuano ya klabu Afrika.